JAPOKUWA imetimia miaka 14 tangu alipotwaa taji la Miss Tanzania mwaka 1999, bado Hoyce Temu anaendelea kuaminika kuwa ndiye mrembo wa mashindano hayo aliyeitumikia jamii zaidi kuliko wengine wote.
Hoyce ambaye kwa sasa anaendesha kipindi cha Mimi Na Tanzania katika Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, amekuwa akijihusisha na jamii ya watu wa chini kwa kuwasaidia kupitia kipindi chake hicho, tofauti na warembo wengi ambao wakimaliza muda wao wa ‘u-miss’, wanaendelea na maisha mengine.
Miaka kadhaa iliyopita wakati aliporejea nchini akitokea Marekani kusoma, Hoyce alifikia katika kituo cha watoto yatima ambapo alikula na kunywa nao.
Katika tukio la kusisimua, kuna siku Hoyce alitembelea Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kumuona mtoto aliyenyonyoka nywele kutokana na ugonjwa huo, mgonjwa huyo alitamka: “Wewe (Hoyce) ni mzuri kwa kuwa una nywele nyingi.”
Kauli hiyo ilimuumiza sana, kesho yake Hoyce alikata nywele kisha akarejea katika taasisi hiyo ili kumpa moyo mtoto huyo, japokuwa baadaye alifariki dunia.
“Nilipokuwa kijijini kwetu Moshi, niliishi maisha ya tabu na shida sana, hivyo ninachokifanya ninakijua, niliishi kwa mlo mmoja na kuchunga ng’ombe, inaniuma sana nikiwaona watu wanaopitia katika maisha hayo, ndiyo maana nimejitolea kuisaidia jamii,” anasema Hoyce ambaye ana umri wa miaka 33.
Hivi karibuni Hoyce ambaye ni Ofisa Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa nchini, alifunga safari hadi Morogoro, Wilaya ya Mvomero katika Kijiji cha Makuyu kwenye familia yenye watoto watano walemavu, bila kujali urembo wake, alikaa pamoja na watoto hao huku akiwasaidia kuwanyanyua na kuwaweka kwenye viti vyao na kucheza nao.
Hoyce aliingia jikoni na kuchochea moto kisha kuwapikia ugali ambao ulikuwa ni mlo wao wa mchana.
Familia hiyo imeeleza kuwa kwa kawaida huwa inapata mlo mmoja kwa siku, huku baba na mama wote wakiwa hawana kazi na wanatumia muda mwingi kuwaangalia watoto wao ambao wote ni walemavu.
“Familia hii ipo kwenye hali ngumu, kwa yeyote atakayejisikia kusaidia, anaweza kufanya hivyo kupitia namba 0713612533, ambapo kwa pamoja tutashirikiana na Global Publishers kufikisha misaada kwa wahusika,” alisema Hoyce.
Hoyce alikulia kwa babu na bibi yake kijijini Old Moshi, Kikarara, akapata elimu ya msingi katika shule za Matemboni, Uhuru, kisha upande wa sekondari alisoma Arusha Sekondari na Zanaki.
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!