StatsCrop - Free website analyzer!

Ads 468x60px

AddToAny

Lorem

Social Icons

August 18, 2012

Mkama:CCM yashikilia urais kutopingwa mahakamani

Tweeted this Like this, be the first of your Friends


Wakati Tanzania ikiendelea kutoa maoni kuhusiana na kuandikwa kwa Katiba mpya, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinaendeleza utamaduni wa matokeo ya urais kutopingwa mahakamani.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Mkama baada ya Tume ya Uchaguzi ya nchini Malawi kutembelea chama hicho kwa lengo la kujifunza jinsi chaguzi za Tanzania zinavyoendeshwa.
Maelezo hayo yamekuja kufuatia swali lililoulizwa na mmoja wa wajumbe wa tume hiyo kutoka Malawi, Mchungaji Maxwell Banda, ambaye alitaka kujua kama CCM kimeridhika na utaratibu wa sasa wa kutopinga matokeo hayo mahakamani.
Mkama alisema kupinga matokeo ya urais mahakamani ni kuifanya nchi kukaa muda mrefu bila Rais wakati ikisubiri hukumu itolewe. Aliongeza kuwa, maamuzi ya kesi kama hiyo huchukua miezi sita au zaidi.
Alitaja moja ya changamoto zilizopo kwenye chaguzi hapa nchini kuwa ni vyama vya upinzani kutoridhika na matokeo pindi yanapotangazwa. “Katika siasa siku zote mshindi huwa haulizi matokeo lakini uzoefu unaonyesha vyama pinzani vimekuwa havikubali matokeo yanayotangazwa,” alisema.
Kuhusu mgombea binafsi, Mkama alisema nchi ambayo haijakomaa kidemokrasia kama Tanzania ni vigumu kwa mgombea huyo kumudu gharama za uchaguzi.

Alisema mfumo wa vyama ni mzuri ikilinganishwa na mgombea binafsi kwa sababu maambuzi hufanywa na watu wengi wakati mtu binafsi hutumia misimamo yake.
Naye Banda alisema mtazamo wa wamalawi kuhusu mgombea binafsi wao huamini kuwa huleta changamoto kwenye vyama vya siasa kutokana na jinsi wanavyoendesha kampeni na kukuza demokrasia.
“Malawi wameruhusu mgombea binafsi kutokana na ukosefu wa demokrasia kwenye vyama na kwa sasa wana wabunge 39 kati ya 193 ambao wanatokana na wagombea binafsi,” alisema Banda.
Mjumbe mwinginewa tume hiyo ya Malawi, Gloria Chingota kwa upande wake alisema wamejifunza mambo mengi kupitia chaguzi za hapa nchini ambazo zitawaongoza kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2014.
Aliongeza kuwa, wataishauri serikali yao kuwa na viti maalum katika bunge lao kama ilivyo hapa Tanzania kwa lengo la kuwajengea uwezo wanawake wao. Pia alisema Tanzania inaweza kujifunza kutoka Malawi jinsi ya kuimarisha demokrasia.

Aidha alisema nchi yake ipo makini katika uchaguzi ambapo mpiga kura anaweza kupiga kura bila ya kuwa na kitambulisho kwa sababu wasimamizi huwatambua kwa picha na majina kupitia vituo vya kupigia kura. Tume hiyo hapa nchini imetembelea Tume ya Uchaguzi nchini (NEC), mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na vyama vya siasa kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF).

0 comments:

Post a Comment

Toa maoni yako hapa!

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
Web Directories
PageHeat