Maandalizi ya MAONYESHO YA ASALI YA DAR ES SALAAM (DAR ES SALAAM HONEY EXHIBITION) ambayo yatafanyika katika
viwanja vya Mwalimu Nyerere (Sabasaba) Dar es Salaam tangu tarehe 3 hadi 7 Oktoba 2012 yamekamilika. Wananchi
wanakaribishwa kuhudhuria maonyesho hayo ambayo hayatakuwa na kiingilio. Katika
maonyesho hayo watu wataelimika kuhusu manufaa yatokanayo na asali, pia watapata
utaalam wa kufuga nyuki na wataonja na kununua asali bora kwa bei nafuu.
Kaulimbiu ya maonyesho hayo
ambayo ni ya kitaifa ni ASALI KWA AFYA NA
USTAWI (HONEY FOR HEALTH AND PROSPERITY).
Maonyesho hayo yameandaliwa kwa
ushirikiano wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara
Tanzania (TanTrade) na wadau wengine wa
Sekta ya Ufugaji Nyuki. Lengo kuu la maonesho ni kuhakikisha upatikanaji wa
masoko ya uhakika ya mazao ya nyuki.
Tarehe 3 Oktoba ni siku iliyotengwa maalum kwa ajili
ya kufanyika Kongamano la Ufugaji Nyuki. Hivyo wafugaji nyuki, wataalam na
wadau mbalimbali wa Sekta hiyo wanakaribishwa kuhudhuria kungamano hilo ambalo
litafanyika katika ukumbi wa J. M. Kikwete ulioko kwenye viwanja vya Mwalimu
Nyerere .
Ufunguzi rasmi wa maonyesho hayo utafanyika tarehe 5
Oktoba 2012 ambapo Mgeni Rasmi
anategemewa kuwa Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo
Peter Pinda (Mb).
Waonyeshaji waliothibitisha kushiriki ni Halmashauri za Wilaya zote, kampuni zinazonunua asali, watengenezaji
wa mizinga na vifaa vingine vya kisasa
vya ufugaji nyuki, na
watengenezaji wa bidhaa zinaotumia asali na nta kama malighafi.
Inategemewa kuwa katika maonyesho
hayo waonyeshaji watajitangaza ili waweze kupata wanunuzi wa asali na mazao
mengine ya nyuki. Pia wanunuzi wa mazao ya nyuki watapata fursa ya kuwafahamu wafugaji.
Aidha inategemewa kuwa utaundwa mtandao ambao utawaunganisha wazalishaji,
wafanyabiashara, wataalam na wadau wa sekta ya nyuki.
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
30 Septemba 2012
Simu:
+255 784 468047
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!