Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
Bodi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, imewasimamisha kazi
madaktari 72 kwa kosa la kutoingia kazini kwa siku tano jambo ambalo ni
kinyume cha makubaliano ya mkataba.
Madaktari hao ni 54 wa
mafunzo ambao waliingia mkataba wa miaka miwili na hospitali ya Rufaa na
Madaktari 18 walioajiriwa na Wizara ya afya.
Akizungumza na
waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Norman Sigara, alisema kitendo cha madaktari kutoripoti kazini kwa siku
tano ni ukiukwaji wa kanuni za utumisha wa umma toleo la 2009 kifungu
namba F.16-F17 na F. 27.
"Hivyo kupitia kanuni hiyo madaktari hao
wamesimamishwa kazi na kurudishwa kwa mwajiri wao ambaye ni Katibu Mkuu
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa hatua zaidi za kinidhamu,"alisema
Sigara.
Imeelezwa kuwa, siku ya tarehe 23/6/2012 wafanyakazi 15
waliokuwa zamu (Intern Doctors 12 na Registrars3) hawakufika kazini na
tarehe 24/6/2012 wafanyakazi 19 (Intern doctors 15 na Registrars 4)
hawakufika kazini.
Alisema, kuanzia tarehe 25/6/2012 imethibitika
kuwa Interns Doctor 54 na Registrars 18 hawakufika kazini hadi leo
tarehe 28/6/2012. Tarehe 25/6/2012, bodi ya hospitali ilifanya kikao cha
dharura kujadili hali ya utendaji kazi na utoaji huduma hospitalini na
kutoa uamuzi.
Sigara, aliyataja maamuzi hayo kuwa ni Mwenyekiti
wa Bodi akutane na madaktari ambao hawakufika kazini ili awasikilize
sababu za kutofika na kujadili namna ya kumaliza matatizo hayo jambo
ambalo madaktari hao waligoma.
Alisema, baada ya madaktari hao
kukaidi ombi hilo, Bodi ya hospitali iliwaandikia barua za kujieleza
kwanini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuvunja mkataba walioingia
na hospitali na pia kukiuka kanuni za kudumu za utumishi wa umma nalo
walilikaidi.
"Iwapo madaktari ambao hawakuripoti au kueleza
sababu za kuridhisha ifikapo tarehe 28/6/2012. kwa kuzingatia kanuni za
utumishi wa Umma, madaktari hao watasimamishwa kazi na kurudishwa kwa
mwajiri wao ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,"
alisema.
Aidha, alisema kuwa kwa ujumla madaktari hao waligomea
barua zote mbili, yaani ya kuitwa kwenye kikao pamoja na ile ya kuwataka
kujieleza hivyo Bodi imechukua hatua za kisheria za kuwafukuza kazi.
Kwa
upande mwingine, Mwenyekiti huyo wa bodi alisema kuwa tayari hospitali
ya Rufaa kwa ushirikiano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, madaktari
watano wamepatikana ili kusaidia huduma kwa hospitali hiyo.
June 29, 2012
Bodi ya Hospitali ya Rufaa Mbeya yawasimamisha kazi Madaktari 72
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget