Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
OFISI ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, imesema hakutakuwapo
tena ucheleweshaji mishahara kwa watumishi wapya kutokana na kufungwa
kwa mfumo wa mawasiliano ya kompyuta kila taasisi ya umma.
Taarifa
hiyo ilitolewa jana na Waziri wa ofisi hiyo, Celina Kombani, wakati
akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma kuhusu maadhimisho ya
siku ya Utumishi wa Umma yanayoadhimishwa leo.
Kombani alisema
mfumo huo utawezesha taarifa za watumishi wapya kufika na kufanyiwa
kazi haraka na ofisi ya utumishi, hivyo kuziwasilisha taarifa zao
hazina kwa ajili ya malipo yao.
Alisema kwa sasa kila taasisi ya
Serikali nchini imefungiwa mfumo huo wa kompyuta, hivyo wanatakiwa
kuingiza taarifa za wafanyakazi wao pale walipo kwa kutumia mtandao.
“Sasa
hivi ukiona mishahara inachelewa basi ujue taarifa za mtumishi
aliyeajiriwa zimechelewa kufika utumishi, kwa kuwa zinatakiwa kufika
kabla ya tarehe 15 kwa ajili ya kupeleka taarifa hazina ili waandae
malipo mwisho wa mwezi,” alisema Kombani.
Mbali na mishahara
kutocheleweshwa, huduma hiyo ya mtandao pia itasaidia kupunguza
malimbikizo ya madeni kwa watumishi wa umma kwa kuwa taarifa za kila
siku za mtumishi zitakuwa zikifika ofisi ya utumishi kwa wakati.
Taarifa
hizo ni pamoja na kupandishwa vyeo kwa wafanyakazi, taarifa za vifo,
kuachishwa kazi, likizo na taarifa za wafanyakazi wanaostaafu.
“Mfumo
huu toka umeanzishwa una miezi saba na umeonyesha mafanikio kwa kuwa
kwa kiasi kikubwa, suala la malalamiko ya malimbikizo mbalimbali ya
watumishi yamepungua ukilinganisha na awali. Tunategemea kuyamaliza
kabisa hapo baadaye,” alisema.
Alisema Serikali imeunda Bodi ya
Mishahara na Maslahi kwa Watumishi wa Umma, ambayo itakuwa na jukumu la
kufanya utafiti juu ya hali ya mishahara ya watumishi wa umma.
Waziri
Kombani alisema bodi hiyo itachunguza mishahara ya watumishi wa umma
wote na kulinganisha na hali ya uchumi na gharama za maisha, itaanza
kazi mwaka huu wa fedha.
Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Utumishi
wa Umma, Kombani alisema kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Kujenga uwezo wa
utekelezaji wa mkataba wa misingi na kanuni za utumishi wa umma na
utawala, ili kuwa nchi inayojimudu kwa maendeleo Afrika’.
Alisema
kama ilivyo kawaida kila mwaka kuadhimisha siku ya Utumishi wa Umma kwa
kufanya maonyesho, mwaka huu hayakuwepo ikiwa ni moja ya utekelezaji wa
mkakati wa Serikali wa kubana matumizi ya fedha za umma.