Ndugu zangu,
Watanzania wengi hatuna mazoea ya kusoma, hata makala za magazetini
ukiachilia mbali vitabu vya taarifa na hadithi. Ndio, tu wavivu wa
kusoma.
Kigong’onda ni aina ya ndege. Ndege huyu ana mdomo mrefu na
anapenda sana kugongagonga mti kwa mdomo wake. Ndivyo anavyojipatia
ridhiki yake.
Lakini, kwa hulka yake ya kugong’onda kila kilicho mbele yake,
basi, hata ukimwekea mti wa chuma porini, kigong’onda atahangaika nao
mpaka damu zimtoke mdomoni. Ni hulka yake. Kiongozi hapaswi kuwa kama
kigong’onda.
Kuna hoja mezani juu ya udhaifu wa JK, imetokea Bungeni. Yumkini,
kama mwanadamu, JK ana mapungufu na udhaifu wake, nani asiye na
mapungufu na udhaifu? Lakini, tukimzungumzia JK kama taasisi ya ’
Urais’, namwona Rais anayejipambanua na waliomtangulia. Ni kwa
kujitahidi kufanya yale yalo nafuu na yenye manufaa kwa nchi
yetu kwenye mfumo dhaifu uliopo.
Wanadamu tunapaswa kuhukumu dhamira ya mtu na si matokeo. Bado
namwona JK kama kiongozi mwenye dhamira njema kwa nchi yetu. Nauona
ujasiri ndani ya JK. Ni ujasiri wa kufanya yale ambayo, hata ndani ya
chama chake hayakuwezekana kufanywa na Mwenyekiti wa chama huko nyuma.
Na bila shaka, kuna wahafidhina ndani ya chama chake wanaomwona JK kuwa
ni dhaifu kwa mantiki hiyo. Kuna wanaoamini, ndani ya CCM, kuwa Rais wa
chama tawala anayekaa na kuongea na wapinzani Ikulu ni Rais dhaifu!
Na hata haya tunayoyashuhudia sasa, yumkini ni matokeo ya dhamira
njema ya JK. Naamini, kwa tunavyoenenda sasa, Tanzania atakayoiacha JK
haiwezi tena kurudi kuwa kama ilivyokuwa kwa Julius Nyerere, Ali Hassan
Mwinyi na Benjamin Mkapa. JK amepanua uhuru wa Watanzania kuchangia
fikra zao bila hofu. Siku zote, hofu haijengi nchi.
Maana, tumefika hapa kutokana na mfumo dhaifu unaozaa Serikali
dhaifu, unaozaa Bunge dhaifu na unaopelekea pia kuzaa vyama dhaifu vya
siasa ikiwamo chama tawala. Na chimbuko lake ni Katiba ya Nchi iliyo
DHAIFU. Ndio, tatizo la nchi yetu ni tatizo la kimfumo.
Ni tatizo lililoasisiwa tangu Awamu ya kwanza ya Urais. Angalia,
Katiba yetu inampa nguvu nyingi sana Rais. Tuna bahati tu hajatokea Rais
anayeamua kuzitumia ipasavyo nguvu hizo.
Nimeona katuni ya ndugu yangu Masoud Kipanya kwenye gazeti la
Mwananchi la jana, Juni 23, 2012. Kipanya alionyesha foleni ndefu ya
wapiga kura Watanzania walio tayari kumpigia kura Rais Dikteta.
Niliogopeshwa na michango ya maoni ya Watanzania juu ya katuni
ile. Wengi walionekana kuikubali hali hiyo. Kuwa kwao kwa hali ilivyo
sasa ni heri kutawaliwa na dikteta kuliko Rais dhaifu!
Inasikitisha na inaogopesha kuona kuwa tumefika hapa. Naamini mimi
na wengine wengi tuliokulia enzi za chama kimoja na Rais mmoja ambaye
ni kila kitu, tusingependa kurudi huko tulikotoka. Nikayasoma jukwaa
moja maoni ya Mtanzania Ludovic Mwijage aliyejaribu kuonyesha ubaya wa
udikteta. Hapo chini nimeweka kitabu cha Mwijage kilicho kwenye maktaba
yangu. Kwa mimi niliyesoma kitabu chake, ningeshangaa kama Mwijage
angeunga mkono hoja ya kumwona JK dhaifu na kutamani Rais Dikteta.
Ukweli, sisi wa ’ Kizazi Cha Azimio’ tuliwaona wazazi wetu wakiishi
katika hali ya hofu na mashaka. Waliishia kunong’ona tu pale walipotaka
kuishutumu Serikali na Rais aliye madarakani.
Mjumbe wa nyumba kumi alikuwa ni mtu aliyeogopewa
sana. Huyu alikuwa ni wakala wa Chama tawala na Serikali. Moja ya
majukumu yake ilikuwa ni kuwatambua, katika nyumba zake kumi, wale wote
waliokuwa na mitazamo tofauti na ya Serikali na Mkuu wa Nchi. Ni wale
walioitwa ’ Wapinga Maendeleo!’. Kuna waliosekwa rumande, kuna
waliofungwa magerezani.
Enzi zile viongozi watu wazima walisimama majukwaani na kusema; ”
We have a One Party Democracy!” Katika dunia hii hakuna ‘ One Party
Democracy’ bali ‘ One Party Dictatorship’. Hata kwenye nyumba mwanamme
ukishaoa huwezi tena kutamka juu ya ‘ One Man Family!’- Na watoto
wakiingia kwenye familia , nao pia wanatakiwa wawe na sauti.
Afrika Rais anategemea sana wasaidizi wake katika kuifanya kazi
yake. Hivyo, mfumo dhaifu huzaa wasaidizi dhaifu pia. Mfano, pale
Bungeni hakukuwa na haja yoyote ya mbunge kutolewa nje kwa kutamka ‘ JK
ni Dhaifu’.
Badala yake, ilikuwa fursa kwa wasaidizi wa JK kujenga hoja za kubomoa hoja za mbunge huyo.
Kumtoa Mbunge nje kumemsaidia zaidi kuwasilisha ujumbe wake na hata
ukaaminiwa na wengi. Maana, swali la hata wasiofutilia vipindi vya
Bunge ni ‘ Kwani huyo Mnyika amesema nini?” Ni yale yale ya Zitto Kabwe
kutolewa Bungeni kwa hoja ya Buzwagi. Nakumbuka kumsikia Mzee Malecela
akisimama Bungeni na kutamka, kuwa dawa ya kidole chenye kansa ni
kukikata!
Malecela na wengine katika CCM walisaidia, kwa kasi ya ajabu,
kumtangaza na kumpa umaarufu Zitto Kabwe. Maana, wengi mitaani walitaka
kukiona kidole hicho chenye kansa kinachokisumbua chama tawala na
kikongwe hapa nchini, CCM.
Na mpaka hii leo, CCM wanarudia makosa yale yale ya jana. Na
kwanini wanarudia? Ni kwa baadhi ya watendaji, kuingiwa hofu na wimbi
hili la mabadiliko, hivyo kutojiamini na hata kufanya yale wanayodhani
yatamfurahisha aliyewateua, kumbe, wanamharibia, na wanazidi kukipaka
matope chapa chao.
Naam, tunaweza kuondokana na mfumo dhaifu kupitia Katiba mpya ijayo. Inawezekana.
Makala hii imeandaliwa na Maggid Mjengwa