MWILI
wa aliyekuwa mhariri mkuu wa Gazeti la Jambo Leo, Willy Edward Obunde,
umezikwa leo nyumbani kwao katika kijiji Morotonga, nje kidogo ya mji wa
Mugumu mkoani Mara.
Mazishi
ya mhariri huyo, yalihudhuriwa na wahariri wa vyombo mbalimbali vya
habari, waandishi wa habari, viongozi wa Serikali wakiongozwa na Mkuu wa
Wilaya ya Serengeti kapteni mstaafu James Ryamungu, viongozi wa vyama
vya siasa, madhebu ya dini, pamoja na wananchi mbalimbali.
Aidha,
mazishi ya mhariri huyo, pia yalihudhuriwa na mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mngeja pamoja Mkuu mpya wa
Wilaya ya Magu, ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, Jacqline
Liana.
Ibada
ya mazishi hayo, iliongozwa na Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisi
ya Mara, Hilkiah Omindo, ambaye aliwataka wananchi kujiandaa kwa kufanya
matendo mema na kumtumikia Mwenyezi Mungu.
Akitoa
salamu kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi na wananchi wa Mkoa wa
Shinyanga, Mwenyekiti wa CCM, mkoani Shinyanga, Khamisi Mngeja, amesema
kuwa waandishi wa habari wamepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mwenzao
ambaye alikuwa ni mchapakazi, mwadilifu na anayefuata maadili na weledi
wa uandishi wa habari.
Willy
Edwar (38), alifariki dunia ghafula akiwa mkoani Morogoro, usiku wa
kuamkia juni 17, mwaka huu, wakati akiwa kwenye semina ya uandishi wa
habari za Sensa ya watu na makazi.