Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
SASA bia wanywe wao. Soda wanywe wao. Sigara wavute wao. Sisi basi.
Ebo! Hivi hapa ndipo mahali pekee ambako serikali inaweza kupata fedha
za bajeti?
Twende kwenye bia. Kama serikali inajali, kwanini isiteremshe bei ya
bia. Ili watu wengi waweze kunywa au watu walewale waweze kunywa bia
nyingi.
Ili kampuni ziweze kutengeneza bia nyingi. Ili kampuni zipate mapato
makubwa. Ili kampuni ziweze kulipa kodi kubwa. Ili serikali iweze
kunufaika kwa kodi kubwa. Kwanini?
Twende kwenye soda. Kama serikali inajali, kwanini isiteremshe bei ya
soda. Ili watu wengi waweze kunywa au watu walewale waweze kunywa soda
nyingi.
Ili kampuni ziweze kutengeneza soda nyingi. Ili kampuni zipate mapato
makubwa. Ili kampuni ziweze kulipa kodi kubwa. Ili serikali iweze
kunufaika kwa kodi kubwa. Kwanini?
Twende kwenye sigara. Kama serikali inajali, kwanini isiteremshe bei
ya sigara. Ili watu wengi waweze kuvuta au watu walewale waweze kuvuta
sigara nyingi.
Ili kampuni ziweze kutengeneza sigara nyingi. Ili kampuni zipate
mapato makubwa. Ili kampuni ziweze kulipa kodi kubwa. Ili serikali iweze
kunufaika kwa kodi kubwa. Kwanini?
Sasa wanywaji hawana hamu tena! Ama serikali inywewe bia; inywe soda na ivute sigara. Au wavitumie wanaovitengeneza.
Huo hapo juu waweza kuonekana kama muweweseko wa wanywaji soda, bia
na wavuta sigara; bila kujua uchumi wa uzalishaji na masoko. Lakini kwa
viwango vyovyote vile, kuna mantiki.
Ukitokea mgomo wa “kunywa” na “kuvuta,” mwezi wa sita wa mwaka wowote
ule, nchi ikiwa chini ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), bajeti
haitasomwa kamwe. Haitakamilika.
Kila mwaka ni bia, soda na sigara; hadi wenye viwanda wakaonya kwamba
mwaka huu wakipandishiwa kodi zaidi ya asilimia 10, hawataielewa
serikali.
Kujaribu kuonyesha “ubunifu,” serikali imekuja na pendekezo la
wanaotaka usajili wa magari kwa utambulisho wa taarifa za mtu binafsi –
majina, labda na picha na chochote kile – kulipa Sh. 5 milioni kwa
miaka mitatu.
Ni yaleyale ya bia, soda na sigara. Serikali inasema itakusanya Sh.
50 milioni katika miaka mitato; kwa kutoza Sh. 5 milioni kwa
atakayetaka urembo.
Hii ina maana serikali imelenga watu 10 tu. Wakilipa milioni 50 kila mmoja, serikali itakuwa imeridhika. Masikini!
Kama serikali inahitaji fedha kwa njia hii, kwanini isitoze Sh.
200,000 kwa mwaka kwa gari kwa maelfu ya magari ya vijana wanaotaka
mbwembwe? Itapata zaidi.
Ukiangalia orodha ya magari binafsi yaliyosajiliwa hadi sasa katika
mfumo mpya, utaona yametoka AAA hadi CAG. Haya ni maelfu ya magari.
Serikali haitaki wanaoyamiliki washiriki.
Kinachoonekana hapa ni kwamba, watunga bajeti wanataka watu wachache
(10), na huenda mafisadi wachafu zaidi, wapate nafasi ya kujitambulisha
kwa mbwembwe.
Kwamba wezi wakubwa, wenye mabilioni ya shilingi ya kusambaza;
mabilioni waliyopora umma wa nchi hii; wapate nafasi ya kuwakoga
wananchi na kuonyesha kwamba wao ni tofauti.
Kwamba mafisadi walioshindikana, sasa wapate nafasi ya kurudi upya
katika umma, kwa kuutisha, kuushangaza, kuukoga na kuudhalilisha kwa
fedha walizowaibia.
Lakini, hata kama kiwango kisingekuwa Sh. 5 milioni, au laki mbili;
wazo lenyewe la mikogo, katikati ya umasikini unaoandama wananchi,
hakika ni la kibwege sana.
Aliyetoa wazo hilo barazani na “wataalam” walioliunga mkono ili kupata Sh. 50 milioni, wamedhihirisha uchovu mchafu.
Hiki ni kiasi ambacho serikali inaweza kupata katika siku nne tu
kutokana na faini kwa makosa ya barabarani katika jiji la Dar es Salaam
peke yake!
Serikali yaweza kupata kiasi hiki katika wiki moja au siku saba, kwa kusimamia kwa makini, ukusanyaji kodi kwenye masoko.
Fedha zinazohitajika ili kukidhi mbwembwe za kifisadi, zinaweza
kupatikana – tena mara kumi au ishirini au zaidi – kwa siku moja tu,
kwa kufuta wilaya moja iliyoundwa kisiasa na isiyo na manufaa kiuchumi
kwa wananchi.
Watunga bajeti hawaoni wezi wanaokwapua madini kweupe. Hawaoni
mafisadi wenye kodi za wananchi kwenye akaunti zao Ulaya. Hawaoni
mabomba yanayovujisha mabilioni ya shilingi kwa njia ya mishahara hewa.
Hawaoni! Hawaoni safari za ndani na nje za watawala zinazokausha
hazina na madarasa ya Ngurdoto yanayokamua walipakodi. Hawaoni dege la
serikali lilalo mafuta kama ibilisi. Hawaoni!
Si busara kupendekeza serikali isitoze kodi kwenye bia, soda na sigara. Bali hoja ni hii:
Kuna muda mwingi na mrefu wa kuandaa bajeti. Kuna vyanzo lukuki.
Kitendo cha serikali kuonekana inakwanyiakwanyia – shika hili shika
lile – dakika za mwisho na katika bidhaa zilezile, ni ushahidi watawala
wanaishi kama wapitanjia.
Na mpitanjia hajengi.