Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda , amesema tukio la kupigwa kwa Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Madaktari Dk Stephen Ulimboka, lina utata na kuongeza kuwa
uchunguzi utakaofanywa na vyombo vya usalama ndio utakao maliza utata
huo.
Pinda aliyasema hayo jana bungeni alipokuwa akijibu swali
lililoulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe,
katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo.
“Mazingira ya tukio
hili bado yana utata mwingi, yanahitaji uchunguzi wa kina, kila mtu
anasema lake, mwingine hili na wengine wanasema Serikali ndiyo
imehusika,” alisema na kuongeza:
“Mimi nasema kama ni Serikali basi tutakuwa ni watu wa ajabu sana, Serikali tufanye ili iweje.”
Pia
Pinda alisema kuwa, Serikali imefanya juhudi mbalimbali ili kuhakikisha
kuwa wanaweza kuokoa maisha ya Watanzania ikiwa ni pamoja na kutumia
hospitali za Lugalo pamoja na matawi yake, kutumia madaktari waliostaafu
na wengine walio wizarani.
“Tumezungumza na wenzetu wa Lugalo ili wananchi waweze kutibiwa katika hospitali hiyo na matawi mengine,” alisema Pinda.
Baada
ya maelezo hayo, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Tundu Lisu,
alimuuliza Pinda kwa nini asiwajibike katika suala la mgomo wa madaktari
kwani ni yeye amekuwa akilishughulikia kwa muda na halionekani kupata
ufumbuzi.
Baada ya swali hilo, Pinda alisema kuwa, yapo mazingira
yanayoweza kumlazimu kuwajibika lakini siyo, haya ya mgomo wa madaktari
kwani amejaribu kwa kiasi kikubwa kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.
“Yapo
mazingira yanayoweza kunifanya nijiuzulu, lakini hili la madaktari
nimejaribu kwa uwezo wangu, lakini be what it is (kwa jinsi lilivyo),
kuna changamoto nyingi katika suala hili,” alisema Pinda.
Baada
ya majibu hayo, Lisu alipewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na
kusema “If you have tried your very best and you failed, why don't you
resign?” (kama umejaribu kufanya kila linalowezekana ukashindwa, kwa
nini usijiuzulu??)
Baada ya swali hilo, Spika Anne Makinda
alimtaka Waziri Mkuu kutojibu swali hilo la nyongeza kwa maelezo kuwa,
linafanana na swali la msingi.
Hata baada ya maelezo ya Spika,
Waziri Mkuu alijibu kwa kumueleza Lisu kuwa, anamuheshimu sana lakini
lugha aliyotumia katika kuuliza swali lake siyo nzuri.
Mbunge
Mwingine aliyezungumzia suala hilo ni Martha Mlata, aliyesema kuna uvumi
kuwa, kuna watu wanawapa baadhi ya madaktari fedha ili wahamasishe
wenzao kugoma.
Alisema kuwa, lengo la kikundi hicho ambacho hakukitaja, ni nchi isitawalike.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema na wao (Serikali) wamesikia uvumi huo na wameviagiza vyombo vya usalama vilifanyie uchunguzi.