Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
WAPINZANI wa Yanga, mabingwa watetezi Kombe la Kagame watajulikana leo
wakati ratiba ya michuano hiyo itakapowekwa hadharani tayari kwa
michuano hiyo itakayoanza Julai 14 hadi 28 kwenye Uwanja wa taifa, Dar
es Salaam.
Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika
Mashariki na Kati, Cecafa, Nicholaus Musonye alisema jana kuwa ratiba
hiyo itakuwa hadharani baada ya timu zote kuthibitisha kushiriki
michuano hiyo.
Yanga inayotetea ubingwa wake, huenda ikafungua
dimba la michuano hiyo. Itasindikizwa na timu za Simba (bingwa Bara) na
Azam iliyoshika nafasi ya pili.
Musonye alisema kuwa michuano
itafanyika kama ilivyopangwa jijini Dar es Salaam na ule wa Azam wenye
uwezo wa kuchukua mashabiki 7,000.
Timu zitakazoshiriki ni APR
(Rwanda), Yanga, Simba, Azam (Tanzania), Tusker (Kenya), Wau Salam
(Sudan ya Kusini) na Atletico ya Burundi.
Timu nyingine ni
Mafunzo (Zanzibar) Mamlaka ya Mapato (Uganda), Elman (Somalia), Ports
(Djibouti), Red Sea (Eritrea) na Coffee ya Ethiopia.
Naye Rais
wa Cecafa, Leodegar Tenga wamemshukuru Rais Paul Kagame kwa jitihada
zake za kuinua soka katika ukanda huo. Rais Kagame amekuwa akidhamini
michuano ya Cecafa tangu 1999.
Musonye aliwataka wadhamini
wengine kujitokeza kusaidia kufanikisha michuano ya 2012 kama
ilivyofanya Supersport ambayo imeahidi kuonyesha 'live' mechi za
michuano hiyo.
Wakati huo huo, Dynamos ya Zimbabwe imetupilia
mbali mwaliko wa Cecafa kushiriki michuano yake kwa kuwa inajiandaa na
mechi za Kombe la Caf dhidi ya Inter-club ya Angola.
Dynamos
itacheza mechi yake kati ya Julai 14 na 16 siku ambayo michuano itaanza.
Mbali na mechi hiyo, pia inakabiliwa na mechi ya ligi dhidi ya Hwange
na Highlanders pamoja na michuano ya Banc ABC Super Eight inayoanza
Julai 21.
Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Ray Kazembe alisema kuwa hawataweza kwenda Tanzania kutokana na majukumu hayo.
Mbali
na timu hiyo, Musonye alisema pia kuwa wanatarajia Vita Club ya DRC
pamoja na Bloemfontein Celtics, Platinum FC na Silver Stars za Afrika
Kusini kushiriki michuano hiyo.
Awali ilielezwa kuwa Orlando
Pirates ilialikwa lakini huenda isije kutokana na majukumu ya ligi
wakati TP Mazembe iliyoalikwa, imechomoa kwa kuwa inabanwa na mechi za
Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Kwa sasa tuko katika mchakato
kuhakikisha tunapata timu tatu kutoka nje ya ukanda wa Cecafa. nafasi ya
timu kuja ni kubwa, na tunapigana kupata timu moja kutoka DR Congo,"
Musonye alisema.
"Madhumuni ya Cecafa kualika timu hizi ni kuipa sura michuano hii kwa kuwa ni mikubwa katika ukanda huu."