Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
ASEMA ATAANIKA KILA KITU BAADAYE, ASEMA ACHWE APUMZIKE, MKUU WA
JOPO LA MADAKTARI WANAOMTIBU ASEMA ALING'OLEWA KUCHA, MENO MAWILI NA
KUPATA MTIKISIKO WA UBONGO
MWENYEKITI
wa Jumuiya ya Madaktari aliyetekwa nyara na kuumizwa vibaya usiku wa
kumkia juzi, kisha kutupwa Msitu wa Pande, Dk Steven Ulimboka amesema
atazungumza kwa kina yote yaliyomsibu baadaye na kuomba sasa aachwe
auguze maumivu makali yanayomkabili.
Dk Ulimboka aliokotwa na
wasamaria wema juzi asubuhi katika Msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la
Dar es Salaam, baada ya kutekwa nyara na watu waliokuwa na silaha akiwa
katika Viwanja vya Klabu ya Leaders, Kinondoni.
Jana, Dk Ulimboka
ambaye amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili huku hali yake ikiwa
haijatengemaa vyema, alitoa kauli akisema ingawa ana maumivu makali
anaendelea vizuri ikilinganishwa na siku ya kwanza.
Dk Ulimboka alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa aeleze mkasa huo uliomfika wa kukamatwa, kuteswa na kutupwa msituni.
DR ULIMBOKA AKIWA ICU
Hata
hivyo, hadi sasa wingu zito la nani alimteka na watekaji walitaka kujua
nini kutoka kwa kiongozi huyo wa madaktari, bado limetanda.
Siri nzito
Akisimulia
mkasa huo kupitia Kituo cha Redio cha Clouds FM, Dk Ulimboka alisema,
akiwa katika klabu hiyo ya Leaders alipigiwa simu na rafiki yake ambaye
alikuwa atokee Tandika na baada ya kumsubiri ndipo alipofika kwenye
klabu hiyo, lakini, alianza kujisikia vibaya tofauti na siku nyingine na
kuongeza; "Yaani sikuwa na amani."
Alisema, "Mara, katikati ya
maongezi tukaona mtu anaongea na simu. Ghafla tukiwa tunasema tuagane,
wakaja watu kama watano hivi na bunduki, wakasema wewe na yule bwana mko
free (huru), tunakuchukua wewe (Dk Ulimboka)," alieleza na kuongeza:
"Sijakaa
sawa, nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na
kuniingiza kwenye gari nyeusi, lakini halikuwa na namba."
Hata
hivyo, jana Dk Ulimboka hakuonana na mwandishi wa habari hii, badala
yake alirekodiwa, na Mwananchi kupata sauti yake akijibu swali kuhusu
hali yake na tukio hilo, baada ya uongozi wa Taasisi ya Mifupa
Muhimbili (Moi) kuzuia watu kumwona.
Daktari huyo wa magonjwa ya binadamu, amelazwa katika chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).
"Kidogo
najisikia nafuu ikilinganishwa na nilivyokuja ingawaje, bado nina
maumivu makali. Kwa hivyo, ingependeza niendelee na mapumziko na mtu
yeyote anayetaka kuniona pengine hilo jambo lisifanyike sasa. Hivi sasa
ni vizuri nipumzike," ilisikika sauti hiyo ya Dk Ulimboka.
Lakini,
uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wodini alikolazwa Dk Ulimboka,
kuna ulinzi mkali wa madaktari na hairuhusiwi watu kumwona kiholela siyo
tu kwa sababu za kutaka aachwe apumzike, bali pia kutowaamini watu
ovyo.
DR ULIMBOKA AKIWA ICU
Madaktari wanaolinda eneo hilo walisikika jana wakisema,
“Huyu tunamlinda wenyewe na haiwezekani mtu asiyefahamika kuingia humu
ndani, na hilo tutahakikisha sisi wenyewe,”alisikika akisema mmoja wa
madaktari hao.
Kiongozi jopo la madaktari
Katika hatua
nyingine, kiongozi wa jopo la madaktari wanaomuhudumia Dk Ulimboka,
Profesa Joseph Kahamba aliwaambia waandishi wa habari kuwa Dk Ulimboka
ana majeraha mwili mzima.
“Ingawa kwa sasa anaendelea vizuri, Dk
Ulimboka ameumia sana, kwani mwili wake mzima una majeraha kutokana na
kupigwa na watekaji hao,”alisema Profesa Kahamba na kuongeza:
“Aliumia
mbavuni,kifuani, miguuni, mikononi ambako aling’olewa baadhi ya kucha
za vidole na kichwani na kinywani, ambako aling’olewa meno
mawili,”alisema.
Alifafanua kwamba, kutokana na maumivu hayo ya
kichwa, Dk Ulimboka alipata tatizo la mtikisiko wa ubongo, lakini
akasisitiza kuwa madaktari bingwa wanaendelea na harakati za kuokoa
maisha yake.
DR ULIMBOKA AKIWA ICU
Uongozi wa Moi watoa neno
Uongozi wa Taasisi
ya Mifupa (Moi) umeeleza kuwa hali yake inaendelea vizuri ingawa bado
amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi cha taasisi hiyo.
Msemaji
wa Moi, Almas Jumaa aliwaambia waandishi wa habari kuwa licha ya hali
yake kuendelea vizuri, lakini haingewezekana kwa waandishi wa habari
kuingia ndani ya chumba alikolazwa na kumwona Dk Ulimboka.
“Mgonjwa
anaendelea vizuri ukilinganisha na jana (juzi), anaongea, anawatambua
watu wanaokwenda kumwona, lakini utaratibu wa kwenda kumwona kwa ninyi
imeshindikana kwa sababu yupo (ICU) ni chumba chenye utaratibu
wake,”alisema Jumaa.
Jumaa aliongeza kwamba ili mtu aweze kuingia
wodini analazimika kuvaa vazi maalumu na mavazi yaliyopo,
yasingetosha, lakini pia wapo watu wanaoendelea kumpatia huduma ya
matibabu.
Tamko la Jumuiya ya Madaktari
Wakati hali ya Dk
Ulimboka ikiwa hivyo, madaktari wameipinga tume ya uchunguzi iliyoundwa
na Jeshi la Polisi kuchunguza suala hilo, wakidai mazingira ya tukio
hayaliondoi jeshi hilo kuhusika.
Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk Edwin
Chitage aliwaambia waandishi wa habari kuwa wangependa kuundwa kwa tume
huru itakayofanya kazi ya kuchunguza tukio hilo na kutoa taarifa kwa
umma.
“Madaktari kwa ujumla wetu tunalaani tukio la kutekwa
nyara,kupigwa na kutupwa katika Msitu wa Pande, lakini pia hatuna imani
na tume iliyoundwa na Jeshi la Polisi kwa sababu mazingira ya tukio
hayaondoi kuhusika ama kutohusika kwa jeshi hilo,”alisema Dk Chitage.
Chitage
alitoa msimamo wa madaktari kuwa ni kuendelea na mgomo, huku akionya
Serikali kuacha vitendo vya kuwatisha, kwa madai kuwa vitendo hivyo
haviwezi kuwa suluhu ya mgogoro kati ya pande hizo mbili.
“Kumekuwa
na vitisho kwa madaktari katika maeneo mbalimbali nchini, hususan
Dodoma, Mbeya, Arusha na Mwanza. Tunaionya Serikali kuacha mara moja na
itambue kuwa mgogoro huo hauwezi kumalizwa kwa namna nyingine yoyote
bali ni kwa Serikali kutekeleza madai ya madaktari,”alisema Chitega na
kuongeza:
“Sisi madaktari kwa umoja wetu, tumechoka kushuhudia
Watanzania wakipoteza maisha kwa magonjwa tunayoweza kuyatibu, kufanya
kazi katika mazingira magumu huku kukiwa hakuna mipango ya kuboresha
mazingira ya kazi, kukosekana kwa dawa na vifaa tiba.”
Mgomo huo wa madaktari leo unaingia siku ya saba tangu ulipotangazwa na mwenyekiti huyo kuwa, ungeanza rasmi Jumamosi iliyopita.