Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Mh. Bernard Membe jana alizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tuhuma za wizi wa kiasi cha Tsh. 3.5billion zinazodaiwa kupotea/kutumika katika mazingira yasieleweka.
Aidha hivi karibuni, SERIKALI imeanza uchunguzi wenye lengo la kubaini kama maofisa wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa walifuata taratibu
kutoa kutoka Hazina Sh3.5 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya safari za
Rais Jakaya Kikwete ndani na nje ya nchi.
Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimatifa, Bernard Membe alisema jana kuwa fedha
zinazochunguzwa ni zile zilitolewa kati ya Machi Mosi na Machi 8, mwaka
huu kwa ajili ya safari za Rais Kikwete kwenda Geneva, Brazil, Adis
Ababa na Arusha.
Wiki iliyopita gazeti moja la kila wiki
liliripoti kuwa maofisa watano wa wizara hiyo wamesimamishwa kazi kwa
tuhuma za kuiba fedha zilizotengwa kwa ajili ya safari za rais kutoka
benki moja nchini.
Fedha zilizotolewa kutoka Hazina ni Sh 3.5
bilioni wakati zilizokuwa zimepangwa kwa safari hizo ni Sh2
bilioni.Fedha hizo zinadaiwa kutolewa Hazina na maofisa waliokuwa
wakikaimu nafasi mbalimbali, katika wizara hiyo.
Waziri Membe
alisema wakati tukio hilo likitokea, yeye, naibu wake, Katibu Mkuu,
Naibu Katibu Mkuu na Mhasibu Mkuu walikuwa safarini na kwamba nafasi zao
zilikuwa zinakaimiwa.
“Waliokuwa wanakaimu wali-process (andaa)
fedha za safari pamoja na hazina, na fedha zikapatikana tarehe 8,”
alisema Membe na kuongeza kuwa;
“Ofisa Masuhuri hakushirikishwa na
uchunguzi wa kamati unaendelea ili kujiridhisha kama taratibu zote za
kiutawala zilifuatwa,” alisema.
Alifafanua kwamba tayari
walifanya uchunguzi uliohusisha Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Usalama wa Taifa na wakaguzi wawili
kutoka wizarani hapo.
“Hakuna tuliyemshuku ama kumuita mwizi kwa
sababu hakuna hata fedha iliyoibwa, zote ziliingia kwenye akaunti ya
wizara na nyingine zililetwa wizarani,” alisema.
Waziri huyo
alisema uchunguzi wa kamati unaoendelea, sasa unalenga kuangalia kama
taratibu zilifuatwa na wale waliokuwa wanakaimu.“Uchunguzi wa kamati
utakapokamilika na kubainika makosa yalikuwa wapi utawekwa hadharani,”
aliahidi.
Utabiri wake Chadema
Akizungumzia taarifa za kuitabiria
Chadema ushindi mwaka 2015, Membe aliwatuhumu watu aliowaita maadui wake
kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema wameshiriki
kumlisha maneno ya kukitabaria ushindi chama hicho kikuu cha upinzani
katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
"Kuna taarifa za mimi
kutabiria ushindi Chadema 2015. Naomba niseme kitu kimoja, kama kuna mtu
anajua mimi niliwahi kufanya utabiri ajitokeze. Mimi siyo TB Joshua wa
Nigeria, mtoto wa marehemu Shehe Yahaya au (jina la kampuni moja ya
kimataifa)...ambao wao kila mara ndiyo hufanya utabiri," alisema Membe
huku akionekana kuchukizwa na taarifa hizo.
Membe alifafanua
kwamba, ni kweli alikutana na ujumbe wa Chadema nyumbani kwake jimbo la
Mtama, mkoani Lindi na kufanya nao mazungumzo, lakini hakuwahi kutabiri
kwamba chama hicho kikuu cha upinzani kingeweza kushinda mwaka 2015.
"Nikweli
nilifanya mazungumzo na Chadema walipokuja jimboni kwangu Mtama. Tena
walikuja bahati nzuri walikuta chakula cha mchana tayari,
nikawakaribisha vizuri. Wapinzani si maadui, yaani watu walitaka
niwafukuze chakula. Najua kuna watu hawakufurahia kuwaalika Chadema kuja
kwangu," alisema Membe na kuongeza;
"Ni kweli niliongea nao.
Niliongea nao mambo matatu, kwanza niliwapongeza kwa kujipenyeza hadi
vijijini. Niliwaambia, ni vema mmetambua umuhimu wa kufika hadi vijijini
maana mwaka 2010 mlilalamika kuibiwa kura wakati vijijini mlikuwa
hamjafika. Lakini pia, nikawambia ni vema wametambua umuhimu wa kuanza
kufanya siasa kwa kujenga hoja na tatu, nikawambia nyie fikeni vijijini
sisi kina Membe hatujaanza kutimua vumbi."
Alifafanua kwamba,
anaamini watu wa Chadema waliokuwapo katika mkutano huo ambao ni pamoja
na Dk Slaa na Lema hawawezi kuzusha taarifa hizo zilizotolewa na
kuongeza, "Nimesoma vizuri Political Science, adui wa kisiasa katika
chama siku zote yumo ndani ya chama hicho. Kwa hiyo hata hili naamini
limetoka kwa baadhi ya maadui ndani ya CCM na kwa Chadema ni maadui wa
Chadema."
Kuhusu APRM
Katika hatua nyingine, Membe alisema
taarifa ya Tanzania kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Kujitathmini wa
Umoja wa Afrika (APRM), itajadiliwa mwakani nchini Addis Ababa.
Licha
ya waziri huyo kukiri kwamba Tanzania inadaiwa dola za Marekani 800,000
za ada, alisema hiyo si sababu ya taarifa ya Tanzania kutojadiliwa
mwaka huu kama ilivyotarajiwa.
Rais Kikwete alitarajiwa
kuwasilisha ripoti ya Tanzania kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja
wa Afrika (AU), utakaofanyika Lilongwe, Malawi Julai 10 mwaka huu,
lakini haitafanyika hivyo.Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti kuwa
Rais Kikwete amezuiwa kuwasilisha taarifa ya Tanzania kutokana na deni
hilo.
“Walitakiwa wajadili taarifa ile halafu walete maswali tujibu ndipo wataandaa taarifa ikajadiliwe,” alisema Membe na kuongeza;
“Watu wa APRM hawajaja, hivyo itajadiliwa katika mkutano wa Addis Ababa mwaka 2013,” alisema.
Tanzania
inadaiwa dola za Marekani 800,000 deni ambalo ni malimbikizo ya ada ya
dola 100,000 kila mwaka, kwa miaka minane mfululilizo tangu mwaka
2005.“Mara kwa mara tumekuwa tukiwakumbusha Hazina kuhusu deni hili na
si kwamba ndilo limezuia,” alisema.
June 19, 2012
Wizi fedha kiasi cha Tsh 3.5 billioni za safari za JK kufanyiwa uchunguzi
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!