VUTA nikuvute baina ya Polisi na Chadema imehamia Iringa, ambako jeshi hilo limezuia maandamano na mikutano yote ya chama hicho iliyokuwa imepangwa kufanyika kwa siku nane kuanzia jana.
Amri hiyo ya polisi imekuja siku moja baada ya kutokea vurugu kubwa mjini Morogoro, baina ya wafuasi wa chama hicho na polisi na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wawili kujeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda alisema jana kuwa wameamua kuzuia maandamano na mikutano ya Chadema iliyopangwa kuanza jana kutokana na Sensa ya Watu na Makazi.
“Kutokana na hali halisi ya Sensa, tumeamua kuzuia maandamano na mikutano yote ya vyama vya kisiasa mkoani Iringa wakiwamo hawa watu wa Chadema,” alisema.
Alisema kabla ya kuwazuia, walikutana na viongozi wa chama hicho Wilaya ya Iringa na kuwataka wazuie mikutano yao, jambo ambalo alisema walilikubali kwa ‘mbinde’.
Dk Slaa: Wametuomba
Awali, akiwa Mjini Morogoro, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema polisi wamekiomba chama hicho kusitisha maandamano na mikutano yake iliyopangwa kufanyika mkoani Iringa kupisha Sensa ya Watu na Makazi.
Alisema Chadema imekubali ombi hilo lililotolewa na Mkuu wa Polisi, IGP Said Mwema hivyo kuamua kusitisha mkutano wake uliopangwa kufanyika katika Viwanja vya Mwembetogwa, Iringa jana.
“Juzi Agosti 27, 1:00 usiku tulipata barua kutoka Jeshi la Polisi Iringa iliyokubali Chadema kufanya maandamano wakiwa ndani ya magari na si matembezi ya miguu, lakini baadaye saa 3:00 usiku, tulipigiwa simu na OCD wa Iringa akitujulisha kuwa maandamano yao yamebatilishwa na kutengua mambo yote tuliyoafikiana mwanzo,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Asubuhi ya leo (jana) tulipigiwa simu na RPC (wa Iringa) na kudai kuwa wanataka kuonana na viongozi wa Chadema, huku wakiwa na hoja kuwa tuahirishe kufanya mkutano kutokana na Sensa.
Hoja nyingine ambayo mimi naona ni ya upuuzi ni ile ya kusema kwamba wananchi wa Iringa watakuwa wameathirika na kifo cha kijana aliyekufa Morogoro,” alisema Dk Slaa.
Alisema baada ya kutokubaliana na hoja hizo, alipigiwa simu na IGP Mwema akimwomba asitishe mkutano na maandamano ya mkoani Iringa kwa kuwa hiyo ni amri kwa vyama vyote vya siasa na si Chadema pekee.
“Nimeongea na IGP leo kwa dakika zaidi ya 40 akisema Dk Slaa sijawahi kukuomba hata siku moja, naomba nikuombe na usinikatalie kati ya siku nne hadi tano kuanzia sasa tumezuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara kutokana na kuwapo kwa Sensa naomba tuelewane,” alisema Dk Slaa akimnukuu IGP Mwema.
Vurugu za Morogoro
Juzi, chama hicho kikuu cha upinzani kilifanya maandamano mjini Morogoro na kuzua taharuki, baada ya kutokea vurugu wakati polisi walipoamua kuyasambaratisha na kusababisha mauaji ya mtu mmoja, Ally Zona (38) mkazi wa Kihonda
Akizungumzia kifo hicho, Dk Slaa alisema chama chake kitashiriki kikamilifu katika mazishi ya kijana huyo kulingana na ratiba ya ndugu wa marehemu.
“Endapo familia itaamua kusoma dua hapa Morogoro na kuzika hapa, tutashiriki kikamilifu. Tumejadiliana na wanafamilia kuna mambo ya msingi tumekubaliana na walichoomba ni kusaidia kusafirisha mwili. Hatutajali itikadi aliyokuwa nayo marehemu,” alisema.
Nchimbi achunguza
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi ametuma kikosi maalumu mkoani Morogoro kuchunguza mauaji ya kijana huyo anayedaiwa kupigwa risasi na polisi katika vurugu hizo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Dk Nchimbi alisema Serikali imesikitishwa na tukio hilo hivyo itahakikisha uchunguzi unafanywa na hatua kuchukuliwa kwa watakaobainika kuhusika.
Alisema polisi walipata taarifa ya kuwapo kwa mtu mwenye majeraha umbali wa mita 300 kutoka eneo la tukio na kwamba wasamaria wema walimchukua na kumpeleka hospitali ambako alifariki dunia.
Aliishutumu Chadema kwa kukaidi amri ya polisi iliyowataka wasiandamane.
UVCCM yalaani
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umekishutumu Chadema ukisema kimehusika na mauaji ya kijana Zona yaliyotokea juzi mjini Morogoro.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela alisema: “Tunatoa pole kwa vijana na wananchi wa Morogoro kwa kuondokewa na kijana wao na tunataka uchunguzi ufanyike haraka ili wajulikane waliofanya kitendo hicho.”
“Haiingii akilini kusema Jeshi la Polisi linahusika wakati wafuasi wa Chadema walikuwa wanaonekana vizuri kwa sare zao halafu wawaache na kwenda kumuua mtu aliyekuwa anaendelea na shughuli zake za uuzaji wa magazeti.”
Habari hii imeandikwa na Nora Damian, Tausi Ally, Habiba Yahya na Lilian Lucas na Clement Sanga.
IGP Said Mwema azungumza na Chadema;
Aidha IGP said mwema hivi punde amezungumza na Dr. Slaa kuhusu kuahirisha mikutano yote ya kisiasa nchini na Chadema imeridhia ombi hilo ambalo litadumu kwa siku 5 kutoka leo sababu kubwa ikiwa ni kupisha shughuli za sensa kukamilika nchi nzima
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!