Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) kinahimiza wanachama wake na wananchi kwa ujumla kujitokeza
kutoa maoni kwa tume ya mabadiliko ya katiba ili taifa lipate katiba mpya.
Aidha, CHADEMA kinatoa
mwito kwa wananchi kuondokana na mtizamo kwamba haiwezekani kutoa maoni ya
katiba mpya bila kwanza kuifahamu kwa kina katiba iliyopo bali waelewe kwamba
mchakato huu unahusu kuandika katiba mpya hivyo jambo la msingi ni wananchi
kujitokeza kwa wingi mbele ya tume ya mabadiliko ya katiba mpya na kutoa maoni
kwa kueleza maudhui ya Tanzania wanayoitaka.
Pamoja na kutoa maoni
kuhusu maudhui ya masuala ya kuzingatiwa katika katiba mpya, CHADEMA kinatoa
mwito kwa wanachama na wananchi kutoa pia maoni kuhusu mchakato wa katiba mpya
ili kuiwezesha tume kuishauri serikali kuendelea kuiboresha sheria ya
mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 ikidhi mahitaji ya kujenga kuaminiana na
muafaka wa kitaifa kwa mawasiliano na mashauriano na wadau mbalimbali.
Pia, CHADEMA
kinatahadharisha kuwa uamuzi wa tume kutoa elimu wakati huo huo ikikusanya
maoni utaathiri mchakato wa katiba; hivyo pamoja na kutoa mwito kwa umma kwenda
kutoa maoni kwa tume, CHADEMA kinaendelea na mpango wake wa kutoa elimu kwa
wanachama na umma kuhusu mabadiliko ya katiba.
Wanachama na wananchi kwa
ujumla wazingatie ratiba ya kukusanya maoni kwenye mikoa minane kuanzia tarehe
2 Julai 2012 hadi tarehe 30 Julai 2012 iliyotangazwa na tume ya mabadiliko ya
katiba katika vyombo vya habari na katika tovuti ya www.katiba.go.tz.
Mikoa hiyo ni Tanga,
Kagera, Dodoma, Pwani, Shinyanga, Manyara, Kusini Unguja na Pemba; na kwa namna
ya pekee CHADEMA kinawakumbusha wananchi wa wilaya za Lushoto, Biharamulo,
Bahi, Mafia, Kahama, Mbulu na Kusini ambapo tume ya mabadiliko ya katiba
itaanzia tarehe 2 Julai 2012 kujitokeza kutoa maoni kuwezesha nchi kupata
katiba mpya.
Izingatiwe kwamba
wajibu wa kisheria wa tume ya mabadiliko ya katiba ni kuyapokea maoni na
maudhui hayo na kuandika ripoti na hatimaye kuyaweka katika muundo wa kikatiba
wakati wa kuandaa rasimu ya katiba.
“Wananchi waelewe
kwamba mchakato wa katiba mpya unahusu hatma ya nchi na maisha ya wananchi, kwa
mfano kwa muda mrefu pamekuwepo migogoro katika jamii mingine kuhusu ardhi na
rasilimali nyingine. Kupitia mchakato wa katiba mpya wananchi watoe maoni juu
ya misingi ya kikatiba ya kushughulikia hali hiyo na kulinda haki za msingi za
binadamu”.
“Aidha, taifa lipo
katika hali tete hivi sasa kutokana na tishio la migomo ya madaktari, walimu na
watumishi wengine wa umma; chanzo kikiwa mgawo usio sawa wa rasilimali za nchi
unaofanyika wakati wa bajeti, huku mamlaka makubwa ya kikatiba ya ugawaji na
usimamizi wa fedha za umma yakiwa kwa Rais na serikali badala ya bunge ambacho
ndicho chombo kikuu cha kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi.
Hivyo,
wananchi wajisikie huru kwenda kueleza maudhui ambayo wamekuwa wakiyasema mara
kwa mara ya kutaka madaraka ya Rais kupunguzwa na pia kuweka misingi muhimu ya
kudhibiti ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa maoni kwenye tume ya
mabadiliko ya katiba.”
Ifahamike kwamba miaka
mitano iliyopita CHADEMA kilisambaza kwa ngazi zake zake za chini za chama
waraka na. 4 wa 2007 kuhusu madai ya katiba mpya ambao ulitoa elimu kwa umma
baadhi ya masuala ya kuzingatiwa juu ya katiba. Katika waraka huo CHADEMA
kilielekeza viongozi na wanachama wake kwamba hoja ya Mabadiliko ya Katiba ya
Nchi iwe ya kudumu katika vikao vya kikatiba vya chama pamoja na mikutano na
wananchi mpaka pale taifa letu litakapokuwa na katiba mpya.
Kwa upande mwingine,
ikumbukwe kuwa CHADEMA kilishawatahadharisha watanzania kuzingatia kwamba marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
katiba yaliyofanyika mwezi Februari 2012 yalikuwa ni ya hatua ya kwanza ya kuwezesha kuundwa
kwa tume shirikishi ya katiba kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi na
kuandaa ripoti na rasimu ya katiba mpya.
Hivyo, ili kuwa na
uhakika na mustakabali wa maoni yanayotolewa, wananchi watoe pia maoni kwa tume
kuhusu mchakato wa katiba na pia kuitaka serikali itoe ratiba ya kufanyika kwa
marekebisho mengine muhimu ya awamu nyingine kuhusu bunge maalum la katiba na
hatua ya kutunga katiba mpya na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha
wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki kabla ya mchakato kufikia katika
hatua husika.
Wakati
huo huo; CHADEMA kinatoa tahadhari kuhusu uamuzi wa tume ya
mabadiliko ya katiba kutangaza moja kwa moja ratiba ya kukusanya maoni ya
wananchi bila kwanza kuwa na ratiba ya kutoa elimu kwa umma kuhusu mchakato wa
katiba, katiba, ukatiba na masuala ya katiba.
Uamuzi wa tume kutoa
elimu wakati huo huo ikikusanya maoni unaweza kuathiri mchakato wa katiba;
hivyo pamoja na kutoa mwito kwa umma kwenda kutoa maoni kwa tume, CHADEMA
kinaendelea na mpango wake wa kutoa elimu kwa wanachama na umma kuhusu
mabadiliko ya katiba na inazitaka ngazi zote za chama kuzingatia waraka na. 3
wa mwaka 2011 kuhusu sheria ya mabadiliko ya katiba na kutoa elimu kwa wananchi
kuwezesha nchi kupata katiba mpya na bora.
Imetolewa
tarehe
1 Julai 2012 na:
John
Mnyika (Mb)
Mkurugenzi
wa Habari na Uenezi