Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
Sakata la meli za mafuta zinazodaiwa
kuwa ni za Iran kupeperusha bendera ya Tanzania kwa lengo la kufanikisha
biashara ya nishati hiyo limezidi kuikoroga serikali ambayo sasa
imezipigia ‘magoti’ nchi wanachama wa Baraza la Umoja wa Mataifa
kusaidia kufanya uchunguzi ili kuthibitisha iwapo kuna ukweli kuwa meli
hizo ni za Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar zimelazimika kuomba msaada huo kwa sababu Tanzania ina uwezo
mdogo wa kufanya uchunguzi na kuthibitisha suala hilo.
Membe alisema iwapo uchunguzi huo utabaini kuwa kweli meli hizo ni za
Iran, Serikali ya Mapinduzi ya Zanziar (SMZ) pamoja na ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania zitachukua hatua ya kuzifutilia mbali meli hizo.
“Hivyo tunahitaji ushirikiano kati ya serikali zetu mbili, serikali ya
Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) kusaidia katika kuthibitisha taarifa
hizi kwa sababu wao wana uzoefu mkubwa wa ‘verification’ wa kukanusha
ama kuthibitisha ya kuwa meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania ni
meli za Iran au la”, alisema Membe.
Alisema Serikali ya Tanzania itahakikisha inafanya utafiti wa kina na wa
kuaminika kwa kushirikiana na nchi za Marekani na za Umoja wa Ulaya ili
kupata ukweli wa meli hizo.
MOJA YA MELI ZA IRAN ZINAZOSAFIRISHA MAFUTA
Membe alisema zipo sababu tatu zinazosababisha kufanyika kwa utafiti huo
ambapo moja ni kwamba wakala wa kampuni ya Philtex ya Dubai ambaye
ameingia mkataba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar amekataa kwamba
meli hizo ni za Iran.
Alisema sababu ya pili ni kwamba Julai 2 mwaka huu Wizara yake
ilipomwita Balozi wa Iran kujadili utata wa meli hizo ili athibitishe au
akanushe taarifa hizo alikataa.
Membe alitaja sababu ya tatu ya kufanya uchunguzi huo kuwa ni kutokana
na kwamba sheria ya kimataifa hasa ya Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa inayozikataza nchi wanachama kuruhusu Iran au meli zake kutumia
jina la nchi kwenda katika maji ya kina kirefu kupakuwa na kupakia
bidhaa zake ili kukwepa vikwazo walivyowekewa.
“Vipo vikwazo vilivyowekwa na jumuiya ya kimataifa hasa Umoja wa
Mataifa kulingana na azimio namba 1929 la mwana 2010 inayozikataza nchi
wanachama wa Umoja wa Ulaya kuruhusu Iran au meli zake kutumia jina la
nchi kwenda katika maji ya kina kirefu kupakuwa na kupakia bidhaa zake
ili kukwepa vikwazo alivyowekewa,” alisema Membe.
Membe aliwaomba Watanzania jambo hili lisizushe mtafaruku ndani ya nchi
na kutetemesha Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar na kuwahakikishia
kuwa litamalizwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Aliongeza kuwa lazima ifahamike Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hazitaki kupuuza taarifa
ya kuwepo kwa meli hizo zinazopeperusha bendera ya Tanzania kwenye maji
marefu na ndiyo maana zimeamua kufanya utafiti wa suala hilo.
Mgogoro huu umezidi kupamba moto hapa nchini hasa baada ya Mbunge
Marekani ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Howard Berman,
kuweleza wazi kuwa kitendo cha kusajiliwa kwa meli za Iran na
kupeperusha bendera ya Tanzania ni kuvunja vikwazo vya kiuchumi vya
Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) dhidi ya Iran.
Berman katika barua yake ya Juni 29, mwaka huu aliyomwandikia Rais
Jakaya Kikwete alieleza masikitiko yake kwamba Tanzania imeruhusu
Kampuni ya Taifa ya Meli za Iran (NITC) kupeperusha bendera ya Tanzania
kwenye walau meli sita na zinatarajiwa kufikia 10 na zimesajiliwa
nchini.
“Kwa kuruhusu meli hizo kuwa chini ya miliki ya NITC na kuendelea
kusafirisha mafuta ghafi ya Iran, kitendo hiki kwa serikali yako kina
madhara ya kuisaidia Serikali ya Iran kukwepa vikwazo vya Marekani na EU
ili ipate mapato zaidi ya kugharimia mpango wake wa kutengeneza silaha
za nyukilia na pia kusaidia ugaidi wa kimataifa,” imesema sehemu ya
barua hiyo kwenda kwa Rais Kikwete.
Kadhalika, alisema inasikitisha kuona kwamba serikali ya Tanzania
imekiuka makubaliano ya pamoja ya jamii ya kimataifa ambayo inafanya
kazi kwa pamoja kutumia njia za amani zikihusisha vikwazo vya kiuchumi
ili kubadili tabia ya Iran ya kuhatarisha amani duniani.
“Kitendo cha kuruhusu meli za NITC kupeperusha bendera ya Tanzania
inatia shaka hadhi ya Tanzania katika jamii ya kimataifa,” inasema barua
hiyo.
Kwa maana hiyo, Berman alimuomba Rais Kikwete kufuta usajili wa meli
hizo zinazopeperusha bendera ya Tanzania, kwani kwa mujibu wa uamuzi wa
Rais wa Marekani, Barrack Obama, wa 13608 ambao aliusani Mei mosi mwaka
huu unajumuisha nchi zote na mashirika yote katika ukiukaji wa vikwazo
dhidi ya Iran kama watakuwa wanaisaidia nchi hiyo kukwepa vikwazo
hivyo.”
Kadhalika, mbunge huyo ameonya kwamba endapo Tanzania itaamua kuziacha
meli hizo kuwa na usajili nchini na kuendelea kupeperusha bendera yake,
basi wao katika Bunge la Marekani hawatakuwa na njia nyingine isipokuwa
ni kutafakari kama bado mipango ya maendeleo baina ya Marekani na
Tanzania kama bado inahitajika.
Hata hivyo baada ya suala hili kuibuliwa na vyombo vya habari, Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iliibuka na kutoa taarifa kuwa kwa
kuzingatia sheria ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (Maritime
Authority – ZMA) iliyoundwa kwa sheria No. 3 ya mwaka 2009 ambayo pamoja
na kazi nyingine inasimamia utekelezaji wa Sheria ya usafiri wa Bahari
Zanzibar ya mwaka 2006 (Zanzibar Maritime Transport Act 2006).
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa SMZ, Hamad Masoud Hamad,
aliwasilisha taarifa yake kwa Baraza la Wawakilishi Julai 2, mwaka huu
akithibitisha kusajiliwa kwa meli 10 za Zanzibar ambazo zinapeperusha
bendera ya Tanzania, lakini siyo za Iran ila zimetokea Malta na Syprus.
Alisema SMZ imetiliana mkataba na kampuni ya PHILTEX ya Dubai kufanya
usajili wa meli za kimataifa (Open Registry). Usajili huu umekuwa
ukifanyika tangu mwaka 2009 na mpaka sasa kupitia Wakala wake imesajili
meli 399 ikiwa ni pamoja na meli za mafuta, makontena, za mizigo ya
jumla na meli za abiria.
Alitaja meli hizo kuwa ni Daisy 81479 Daisy Shipping Co. Ltd Malta;
Justice 164241 Justice Shipping Co. Ltd Cyprus; Magnolia 81479 Magnolia
Shipping Co. Ltd Malta; Lantana 81479 Lantana Shipping Co. Ltd Malta;
Leadership 164241 Leadership Shipping Co. Ltd Cyprus; Companion 164241
Companion Shipping Co. Ltd Malta; Camellia 81479 Camellia Shipping Co.
Ltd Malta; Clove 81479 Clove shipping Co. Ltd Malta; Courage 163660
Courage Shipping Co. Ltd Cyprus; Freedom 163660 Freedom shipping Co. Ltd
Cyprus na Valor 160930 valor Shipping Co. Ltd. Cyprus.
Waziri huyo alisema walimtaka wakala wao Philtex Corporation kuwaita
wenye meli hizo na kuwataka kujieleza kuhusu uhusuiano wao na Serikali
ya au makampuni ya mafuta ya Iran na walisema kuwa hawana uhusiano na
Serikali au mamlaka yoyote nchini Iran na wameamua kuja kusajili meli
Zanzibar kwa ridhaa yao.
Jana katika sehemu ya habari kuhusu meli hizi tulisema kuwa Waziri Hamad
alisema Barazani kuwa meli hizo ni za Iran. Tunasikitika kwa upungufu
wa aya hiyo katika habari yetu ya jana. Mhariri.
July 6, 2012
SAKATA LA MELI ZA IRAN KUPEPERUSHA BENDERA ZA TANZANIA
Millionfortune.com
SIASA
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!