Meneja
wa Kitengo cha Habari na Ushauri, HakiElimu, Nyanda Shuli (kushoto)
akijibu maswali anuai ya wanahabari katika mkutano huo.
Meneja wa Kitengo cha Habari na Ushauri, HakiElimu, Nyanda Shuli akifafanua jambo kwa waandishi wa habari.
Mkutano ukiendelea na wanahabari.
Na Joachim Mushi, Thehabari.com
Tasisi
ya HakiElimu nchini imeishauri Serikali pamoja na Chama Cha Walimu
Tanzania (CWT) kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo, ili kumaliza
mgomo uliopo kwani waathirika zaidi na mgomo huo si wao bali ni ni
wanafunzi.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa
HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake kuhusiana na mgomo wa walimu unaoendelea maeneo
mbalimbali nchini.
Alisema
kila mwanafunzi ana haki ya kujifunza na kuelimishwa, kitu ambacho
hawakipati kwa sasa kutokana na mgomo wa walimu wanaoshinikiza Serikali
iwaongeze mishahara pamoja na kuwaboreshea mazingira ya kazi zao.
Mkurugenzi
huyo alisema kauli ya Serikali kudai haina uwezo wa kuboresha maslahi
na mazingira ya kazi ya watumishi wake haileti unafuu wa maisha kwa
watumishi wa umma hivyo kushauri iangalie namna ya kufanya kumaliza
mgogoro huo.
“HakiElimu
inasisitiza kwamba nchi itafanikiwa kuboresha elimu endapo tu itawekeza
kwa walimu kwa kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya walimu,
kuwashirikisha walimu katika maamuzi kuhusu masuala ya elimu na kuwapa
walimu mafunzo kazini. Elimu bora haiwezi kuletwa na walimu walio hoi,”
alisema Missokia.
Aidha
amewataka walimu kuhakikisha wanadai haki zao huku wakiendelea
kuwajibika kwa kufundisha na kuendeleza elimu yetu, kwani wanamgogoro na
Serikali na wala si wanafunzi na jamii kwa ujumla.
“HakiElimu
inawakumbusha walimu kuwajibika. Wadai haki zao, huku wakitimiza wajibu
wao wa kufundisha na kuendeleza elimu yetu. Wafundishe kwa bidii bila
kinyongo, kwa kuwa wasipowajibika watakuwa wanawaumiza wanafunzi na
jamii kwa ujumla. Mgogoro uliopo ni baina yao na Serikali, na si
wanafunzi,” alisema Mkurugenzi huyo Mtendaji.
“Viongozi
wa Serikali wasiwabeze walimu; kwa kufanya hivyo wanawakatisha tamaa.
Hata kama baadhi ya walimu hawakusoma kwa miaka mingi kama ilivyo kwa
fani nyingine, wana umuhimu mkubwa sana. Ndio wanaowaandaa watanzania wa
leo na kesho kimtazamo na kimaarifa. Hivyo, kudai kuboreshewa mazingira
ya kazi ni haki yao; na Serikali inaweza kutimiza wajibu wake kwa
kuwasikiliza na kushauriana nao bila ubabe na kejeli,” alisema.
Pamoja
na hayo ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia
kati mgogoro huo na kutenga muda kujadili suala hilo kwa kina ikiwa ni
pamoja na kuishauri serikali, hasa kuhusu tahadhari za kuchukua ili
tatizo kama hili lisitokee tena.
“Bunge
lina wajibu wa kuishauri na kuisimamia Serikali kuhusu sera, utendaji
na usimamizi wa elimu nchini. Inasikitisha kwamba Bunge linakwepa
kujadili tatizo hili kwa maelezo kwamba liko mahakamani. Tunaamini
kwamba mahakama italiangalia suala hili na kutenda haki, lakini wajibu
wa Bunge uko pale pale…” alisema Bi. Missokia.
Amekiri
kwamba ni kweli gharama za maisha zinazidi kupanda, huku mfumuko wa bei
nao unaendelea kuwaumiza watumishi kila siku, hivyo kuishauri Serikali
kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ili kuweza kuwaboreshea mapato
watumishi wake.
“Serikali
ijijengee utaratibu wa kuboresha mazingira ya watumishi wake, na si
kusubiri kwenda mahakamani kuzuia watumishi kugoma. Watumishi wa umma
watafanya kazi kwa ari endapo tu wameridhika na mazingira ya kazi na
maslahi yao; na si kwa kutumia uamuzi wa mahakama peke yake.”
Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!