Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
Brandts wa pili kutoka kulia, akiwa na viongozi wa Yanga. Kulia ni Seif Magari. Kushoto kwake ni Bin Kleb na Majjid
Anapakia mizigo kwenye gari la Bin Kleb
Anazungumza na Waandishi wa Habari
Akiwa na viongozi wa Yanga
Kulia kwake Bin Klerb, kushoto Mwalusako
Anatoka Uwanja wa Ndege
Millionfortune Dar es salaam,
KOCHA mpya wa Yanga, Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus Johannes Brandts, beki wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi na klabu ya PSV Eindhoven ya Holanzi, amewasili usiku huu (saa 3:45) katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na ndege ya KLM tayari kusaini mkataba na kuanza kazi katika klabu hiyo.
Brandts amepokewa na Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako na viongozi wengine, Abdallah Ahmad Bin Kleb, Seif Ahmad ‘Magari’ na Majjid Suleiman na amesema anaijua Yanga ni timu nzuri, kubwa hana shaka ataiwezesha kufanya vizuri katika medani ya soka Afrika.
Yanga, imetimiza malengo yake ya kuwa kocha mpya, kabla ya kucheza na wapinzani wao wa jadi, Simba SC, Oktoba 3, mwaka huu baada ya kumfukuza Mbelgiji, Tom Saintfiet, kutokana na kuwasili makubaliano na Brandts, ambaye ataanza kazi mara moja kesho.
Mholanzi huyo aliyefukuzwa APR ya Rwanda baada ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Agosti mwaka huu amepewa ukocha wa Yanga, baada ya Mbrazil Marcio Maximo kukataa nafasi hiyo kwa mara ya pili.
Mtaalamu huyo, alizaliwa Februari 3, mwaka 1956 mjini Nieuw-Dijk, Gelderland, mbali na PSV Eindhoven, alichezea pia Roda JC Kerkrade, MVV Maastricht na De Graafschap.
Brandts aliichezea mechi 28 timu ya taifa ya Uholanzi na kuifungia mabao matano na pia alicheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978.
Katika fainali hizo, Raundi ya pili kwenye mechi na Italia, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyezifungia mabao timu zote katika mechi moja kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Alianza kujifunga dakika ya 18, kisha akaisawazishia Uholanzi dakika ya 50 katika mechi ambayo, mchezaji mwenzake Arie Haan baadaye aliifungia timu yake bao la ushindi na kutoka kifua mbele kwa mabao 2–1.
Alipostaafu soka akawa kocha na katikati ya msimu wa 2007–2008, Brandts aliambiwa hataongezewa mkataba NAC-Breda, licha ya matokeo mazuri ya kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie), ingawa uamuzi huo haukuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo na nafasi yake akapewa Robert Maaskant kuanzia msimu wa 2008–2009.
Akateuliwa kuwa Kocha wa Rah Ahan mwaka 2009, kabla ya kufukuzwa Desemba 2009 na kuibukia APR ya Rwanda mwaka 2010, ambako ‘riziki’ yake imeisha miezi miwili iliyopita na sasa amepata maisha mapya Yanga.
Akiwa APR, Brandts alifungwa mechi zote mbili na Yanga iliyokuwa ikifundishwa na Mbelgiji Tom Saintfiet katika Kombe la Kagame, moja ya makundi 2-0 na nyingine ya Nusu Fainali 1-0. Yanga iliibuka bingwa, ikiifunga Azam FC 2-0 kwenye fainali.
Brandts atakutana na wachezaji wake wa zamani wawili Yanga, beki Mbuyu Twite anayeanza msimu wa kwanza katika klabu hiyo na kiungo Haruna Niyonzima anayeingia katika msimu wa pili, ambao alifanya nao kazi APR.