Kituo cha ITV kupitia Twitter kimesema mwenyekiti wa jumuiya
ya madakatari Dr. Stephen Ulimboka ametekwa na kupigwa na watu wasiojulikana na
anapelekwa katika hospitali ya mifupa ya Moi.
Kwa mujibu wa mtandao wa Jamii Forums Dr. Ulimboka ametekwa
majira ya saa sita usiku na watu watatu waliokuwa na silaha za moto na
kumpeleka kusikojulikana! Inasemekana alipigiwa simu na jamaa mmoja
aliyejitambulisha kwa jina moja la 'Abeid' ambaye tangu mwanzo amekuwa
akiwasiliana naye na kujiita afisa wa serikali na kudai kuwa alitaka aonane
naye face to face kwa ajili ya mazungumzo.
Dokta huyo aliokotwa akiwa na hali mbaya sana na hawezi
kuzungumza.
Tukio hilo limetokea wakati kumekuwepo na mgomo wa madaktari
nchi nzima ambao hata hivyo wameonekana kusalitiana kwa kutokuwa na msimamo wa
pamoja, kwani maeneo mengine yote huduma zimeendelea kama kawaida, isipokuwa
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Madaktari hao wametangaza mgomo usio na kikomo kwa lengo la
kuishinikiza serikali kutimiza mahitaji yao, ikiwemo kuboresha mazingira ya
kufanyia kazi pamoja na kuwapandishia mishahara.
Licha ya mgomo huo kuanza kuleta madhara kwa wagonjwa katika
siku ya kwanza juzi, kwa madaktari kutofanya kazi katika hospitali mbalimbali
nchini, jana hali hiyo ilikuwa tofauti kwani sehemu nyingi huduma ziliendelea
kutolewa kama kawaida.
Source: Ipp Media