ALIYEKUWA
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk Asha-Rose
Migiro(pichani) ambaye anarejea nchini leo ametoa waraka maalumu akisema
mwisho wa utumishi wake katika umoja huo ni mwanzo utekelezaji wa
majukumu mengine hapa nchini.
Kauli
ya Dk Migiro imekuja kipindi ambacho jina lake limekuwa likitajwa
katika nafasi ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete atakapomaliza muda wake wa
kuongoza taifa mwaka 2015. Kabla ya kwenda UN, Dk Migiro alikuwa Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Dk
Migiro ambaye aliteuliwa na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-Moon kushika
mwaka 2007 wadhifa huo, alisema anafurahi kumaliza miaka mitano kwa
mafanikio.
Katika
waraka huo ambao gazeti hili limeuona jana, Dk Migiro alisema: “Hakika,
kila chenye mwanzo hakikosi mwisho na kila mwisho wa jambo moja huwa
mwanzo wa jingine.”
Alisema
ingawa ni mapema kwake kutoa tathmini halisi ya utendaji wake kazi,
wadhifa huo katika Umoja wa Mataifa umempatia uzoefu mkubwa.
“Kukitumikia
chombo hiki cha kimataifa kwa muda wa miaka mitano na nusu mfululizo ni
heshima ya pekee ambayo daima nitaienzi kama kilele kimojawapo cha
mafanikio katika maisha yangu ya utumishi wa umma. Kila siku
niliyoitumia katika Umoja huo ilikuwa ni darasa la kusukuma mbele mipaka
ya ujuzi na elimu,” alisema Dk Migiro.
Alisema
amefahamu mambo mengi kuhusu umoja huo, dunia na watu wake ikiwamo
ukomo wa umoja huo katika kushughulikia matatizo mbalimbali
yanayoikabili dunia.
“Daima
nitaendelea kushukuru na kuthamini kwa dhati jinsi Rais Jakaya Mrisho
Kikwete, Serikali na Watanzania wenzangu walivyonitia moyo na kunienzi
katika kipindi chote nilichokuwa Umoja wa Mataifa,” alisema.
Dk
Migiro alisema utumishi wake katika umoja huo ulikuwa fursa adhimu
iliyompa uzoefu wa kipekee hasa ikizingatiwa kwamba aliingia wakati
ukikabiliwa na changamoto kubwa zikiwamo za maradhi, umaskini wa
kupindukia na vitendo vya kikatili na udhalilishaji wa wanawake na
watoto.
Alisema
matatizo hayo na mengine yalimpa fursa ya kuchangia kikamilifu jinsi ya
kukabiliana nayo wakati akitekeleza majukumu yake.
Dk
Migiro alisema umoja huo umemwezesha kufahamiana na viongozi wengi wa
kimataifa na watu mbalimbali wenye mafanikio duniani.... “Nimeweza
kufahamu kwa undani thamani ya michango yao katika kujenga amani na
ustawi wa dunia."
Alisema
ingawa muda wake wa utumishi umekwisha kwenye umoja huo, ataendelea
kuunga mkono jitihada za UN za kukabiliana na changamoto mbalimbali
zinazoikabili dunia.
Sitasahau
Akizungumzia
mambo aliyowahi kukutana nao katika utumishi wake, Dk Migiro alisema
hatasahau hisia alizozipata kila alipokutana na watu wanyonge waliokuwa
wanahitaji msaada wa Umoja wa Mataifa.
“Nitakumbuka
daima tabasamu la mwanamke mmoja niliyekutana naye katika moja ya ziara
zangu barani Afrika nilipotembelea zahanati mojawapo kati ya kadhaa
zinazofadhiliwa na Umoja wa Mataifa,” alisema na kuongeza:
“Mama
huyo mwenye watoto sita, alikuwa amekikumbatia kitoto chake kimoja
kilichokuwa na afya dhaifu kwa kuumwa lakini alikuwa na tabasamu
iliyojaa faraja na matumaini kwa kuwa alikuwa amefanikiwa kupata bure
dawa za kunusuru maisha ya mwanawe.”
Alisema
mama huyo pamoja na matatizo aliyonayo ya kuuguliwa na mwanaye, alipata
faraja baada ya kuwa na uhakika wa kupata matibabu kwenye zahanati hiyo
ya UN.
Dk
Migiro alisema katika utekelezaji wa majukumu mengine, nguvu nyingi
zilielekezwa katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs)
na mengine yaliyokubaliwa kimataifa.
“Nilihamasika
sana na dhamira waliyoionyesha wadau na washirika wetu wa maendeleo,
zikiwemo Serikali, mashirika ya kiraia na mashirika ya biashara katika
kufikia malengo ya milenia,” alisema.
Alisema
anamaliza kipindi chake kukiwa na maendeleo mazuri yanayotokana na
jitihada za kimataifa za kupambana na umaskini akisema mikakati ya UN ya
kutaka kupunguza idadi ya watu maskini duniani kufikia angalau nusu ya
viwango vya sasa, zimeanza kuzaa matunda.
“Taarifa
hii ni ya kutia moyo licha ya ukweli kwamba dunia inapitia matatizo
makubwa ya kiuchumi kuliko wakati mwingine wowote uliowahi kutokea
katika miaka ya hivi karibuni,” alisema Dk Migiro katika waraka wake.
Dk
Migiro alisema wakati wa utumishi wake katika umoja huo, ametumia nguvu
kubwa na hadhi ya ofisi yake katika kupaza sauti za wanawake na
wasichana ili kuleta usawa wa kijinsia.
“Tumeendesha
kampeni za kupiga vita ukatili kwa wanawake na wasichana. Tumezihimiza
mamlaka katika ngazi za kitaifa na kimataifa kutunga sera na sheria
zinazozingatia haki za wanawake na usawa wa kijinsia na tumetaka wapewe
fursa kushika nafasi za uongozi katika jamii,” alisema.
Alisema
ili kufanikisha hilo, umoja huo ulifikia uamuzi wa kuanzisha idara ya
umoja wa mataifa kwa madhumuni ya kuongoza masuala ya wanawake na
masuala ya kijinsia.
“Tumefanya
jitihada hizi kwa kuamini kuwa hakuna uamuzi wowote ule, uwe mdogo au
mkubwa, unaofanywa na Umoja wa Mataifa bila ya kuzingatia maendeleo na
ustawi wa wanawake na wasichana,” alisema.
Alisema
katika eneo la afya ambako wanawake na watoto ndiyo wanaathirika
wakubwa, juhudi zinafanywa kupunguza vifo na kuhakikisha kwamba kila
mwanamke na mtoto anakingwa na maradhi ikiwamo kuzuia maambukizi ya
Virusi Vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Alisema
mwaka 2011, akiwa katika ziara jijini Nairobi, Kenya na Katibu Mkuu,
Ban Ki-Moon walipata fursa ya kukutana na mwanamke aliyeathirika na
Virusi vya Ukimwi ambaye alijifungua watoto pacha watatu waliozaliwa
bila ya kuambukizwa.
Tulifurahishwa
na mpango wa kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama
kwenda kwa mtoto yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa,” alisema Dk Migiro.
Alisema
umoja huo umekuwa ni mtetezi wa wanyonge na wenye kutaabika sehemu zote
duniani na kwamba watumishi wake wanafanya kazi katika mazingira
hatarishi kwa sababu hivi sasa bendera ya bluu si kinga tena akisema
baadhi yao wamekuwa wakiuawa katika matukio mbalimbali.
“Bendera
ya buu haituhakikishii usalama kwani wengi wa watumishi wetu mahiri
wamekuwa waathirika wa matukio ya kikatili ya ugaidi. Nilishuhudia tukio
la aina hii huko Abuja, Nigeria ambako watumishi wenzetu walipoteza
maisha kutokana na shambulio la kigaidi la Agosti 26, 2011,” alisema.
Alisema
mara nyingi watumishi wa umoja huo wanapopoteza maisha, familia zao
zinaachwa katika hali ngumu na kwamba kabla hajamaliza muda wake
alianzisha mchakato wa kubaini namna bora ya kuwasaidia waathirika wa
majanga hayo pamoja na familia zao
Chanzo - http://www.mwananchi.co.tz
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!