Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
Leo tarehe 03 Agosti 2012 kwa mujibu wa Kanuni ya 68 (7) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge na kwa kuzingatia kuwa marekebisho yamefanyika kwenye
ratiba ya bunge ambapo Mkutano wa Bunge sasa umepangwa kuahirishwa
tarehe 16 Agosti 2012 na hoja za wabunge zimeondolewa kwenye ratiba.
Nimeomba muongozo ama Serikali itoe kauli bungeni ya kutengua tangazo
lililotolewa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya
Jamii (SSRA) ili kuwezesha mafao ya kujitoa kuendelea kutolewa au
uongozi wa Bunge uruhusu niwasilishe muswada binafsi wa sheria kwa hati
ya dharura tarehe 16 Agosti 2012 kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye
sheria husika ili kuruhusu mafao ya kujitoa kuendelea kutolewa.
Pamoja na hatua hiyo ya kuomba muongozo nimechukua hatua ya ziada ya
kumwandikia Katibu wa Bunge kumweleza kusudio la kuwasilisha Muswada
Binafsi juu ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social
Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 kwa hati ya dharura kwa
mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka
2007).
Lengo la Muswada huo ni kufanya marekebisho yenye kuwezesha kurejeshwa
kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits) ili kuruhusu kuendelea kutolewa
kwa mafao kwa mwanachama wa mfuko ya hifadhi ya jamii anapoacha kazi na
kuhitaji kupewa mafao yake kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kwa
hiari (miaka 55) au kwa lazima (miaka 60) au pale anapopata ulemavu wa
kudumu.
Nimeomba kupatiwa ushauri na usaidizi wa kisheria kwa mujibu wa Kanuni
ya 21 (1) (d), (e) na (2) ili kuweza kuandaa Muswada Binafsi wa Sheria
kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (1), Taarifa ya Muswada huo kwa mujibu wa
Kanuni ya 81 (2), hati ya kuwasilisha muswada kwa dharura na hoja ya
kutengua masharti kuhusu muda wa utangazaji wa Miswada ya Sheria kwa
mujibu wa Kanuni ya 81 (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka
2007).
Kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (5) masharti kuhusu muda wa utangazaji wa
Miswada ya Sheria yanaweza kuwekwa kando na kutenguliwa kwa hoja
kutolewa na kuamuliwa kama kutawasilishwa Bungeni hati iliyowekwa saini
na theluthi mbili ya Wajumbe wote wa Kamati kama ni Muswada wa Kamati na
kwa Muswada wa Mbunge hati iliyowekwa saini na Wabunge wasiopungua kumi
inayoeleza kuwa muswada binafsi uliotajwa katika hati hiyo ni wa
dharura.
Naomba kutoa taarifa kwamba kuanzia jumatatu tarehe 6 Agosti 2012
nitaanza kukusanya saini za wabunge wanaounga mkono kuwasilishwa kwa
muswada tajwa kwa hati ya dharura kufanya haraka marekebisho yenye
kuwezesha kurejeshwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits) ili
kuruhusu kuendelea kutolewa kwa mafao kwa mwanachama wa mfuko ya hifadhi
ya jamii.
Nimeomba pia kwa Katibu wa Bunge kwa mujibu kifungu cha 10 cha Sheria ya
ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Cap 296 R.E 2002 kupatiwa nakala ya
taarifa na nyaraka zifuatazo kwa ajili ya kujiandaa kuwasilisha muswada
husika: Social Security Ammendment Act no.5 ya mwaka 2012, Sheria za
Hifadhi ya Jamii zinazohusika, Taarifa na mapendekezo yaliyowasilishwa
na kupelekea kufutwa kwa mafao ya kujitoa (withdrawal benefits) na
maelezo kuhusu hatua ambayo kifungu husika kiliingizwa na hatimaye
kupitishwa na Bunge tarehe 13 Aprili 2012.
Pamoja na kuomba taarifa na nyaraka kupitia kwa Katibu wa Bunge natoa
mwito kwa wadau wa mifuko ya hifadhi ya jamii kutunipatia maoni na
mapendekezo kwa ya kuzingatiwa kwenye Muswada Binafsi wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social Security
Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 katika kipindi cha wiki moja.
Ikumbukwe kwamba kifungu cha kufuta mafao ya kujitoa kilichozua mgogoro
hakikuwepo wakati muswada uliposomwa kwa mara ya kwanza bungeni tarehe 1
Februari 2012 bali kiliwasilishwa kupitia jedwali la marekebisho ya
Wizara lililowasilishwa tarehe 13 Aprili 2012 bila malengo na madhumuni
yake kuelezwa kwa ukamilifu.
Kupitishwa kwa kifungu hicho kumethibitisha maneno niliyoyatoa bungeni
kuwa tumefika hapa tulipo kutokana na ‘uzembe wa bunge na wabunge’ na
kwa hili pamoja na mchango nilioutoa bungeni kwa maandishi siku hiyo juu
ya haja ya kuwa mfumo mpana zaidi wa pensheni na hifadhi ya jamii
(universal pension and social security) pamoja na kuwa sikuunga mkono
kifungu husika kilichoingizwa kinyemela naomba radhi kwa wananchi wa
Ubungo na wafanyakazi kwa kutokuwasilisha jedwali la marekebisho kupinga
kifungu hicho kuingizwa.
Izingatiwe kuwa ili kurekebisha hali hiyo tarehe 27 Julai 2012 kwa
nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwa niaba ya Kambi
Rasmi ya Upinzani niliitaka Serikali itoe maelezo maelezo kuhusu taarifa
zilizotolewa bungeni tarehe 13 Aprili 2012 kuwa wafanyakazi ikiwemo wa
migodini kupitia vyama vyao walihusishwa kutoa maoni yaliyopelekea
kufutwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits); suala ambalo Chama Cha
Wafanyakazi wa Migodini (TAMICO) kililikanusha.
Hata hivyo, Waziri wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya Hotuba
yake tarehe 28 Julai 2012 hakutoa majibu yoyote bungeni kuhusu suala
hilo hali ambayo imesababisha migongano kuendelea katika migodi
mbalimbali kuhusu madai hayo hali ambayo kwa taarifa nilizozipata tarehe
1 na 2 Agosti 2012 inaweza kusababisha migomo migodini. Kufutwa kwa fao
la kujitoa kumelalamikiwa pia na wafanyakazi na wadau wa hifadhi ya
jamii katika Jimbo la Ubungo na katika taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, suala hili na tukio husika litumike kama rejea ya bunge na
wabunge kuikatalia Serikali kuwasilisha marekebisho yenye athari kubwa
kipindi cha mwisho na hivyo wabunge kukosa fursa ya kupata maoni ya
wananchi na pia Serikali itakiwe kuomba radhi kufuatia kulipotosha bunge
kuwa wadau wa hifadhi ya jamii hususan wafanyakazi na vyama vyao
walishirikishwa na kuridhia wakati ambapo wamejitokeza na kukanusha
madai hayo yaliyotolewa na Wizara bungeni.
Kwa upande mwingine kufutwa kwa mafao ya kujitoa msingi wake haupo
kwenye marekebisho ya sheria yaliyofanyika tarehe 13 Aprili 2012 pekee
bali ni udhaifu katika mfumo mzima wa kisera na kisheria wa hifadhi ya
jamii nchini hali ambayo inahitaji wadau kutaka mabadiliko makubwa.
Hivyo, naungana na wote wenye kutaka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa
Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kutengua taarifa kwa umma iliyotolewa
ya kueleza kuwa “kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria hiyo (ya 13 Aprili
2012) maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita
hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuwezesha Mamlaka na Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa Wadau”.
Aidha, pamoja na Mamlaka kueleza kwamba sitisho la fao la kujitoa si
kwa sababu za Kiserikali au Mifuko kufilisika ni vizuri mamlaka ikaeleza
kwa uwazi na ukweli sababu zingine za kufanyika kwa marekebisho hayo
zaidi ya ile ya kutimiza malengo ya Hifadhi ya Jamii ambayo ni
kuhakikisha kuwa Mwanachama anapostaafu anapata mafao bora
yatakayomwezesha kumudu hali ya maisha ya uzeeni. Tahadhari za Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika taarifa za Hesabu za mwaka
2010/2011 na miaka mingine zinaashiria masuala ya ziada ambayo yanaweza
kuwa yameisukuma Serikali kuja na mbinu zingine za kuhakikisha uendelevu
wa mifuko ikiwemo kupitia marekebisho ya sheria za hifadhi ya jamii.
Ili bunge liweze kutimiza wajibu wa kuishauri na kuisimamia serikali
kufanya marekebisho yanayostahili ya sheria husika kwa haraka ni muhimu
ratiba ya bunge ikabadilishwa.
Tafsiri ya marekebisho ya ratiba yaliyofanyika ni kuwa hoja binafsi
niliyoiwasilisha kwa katibu wa Bunge kutaka bunge lijadili na kupitisha
maazimio ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa majisafi na
ushughulikiaji wa majitaka haitapata nafasi ya kujadiliwa bungeni. Aidha
ratiba hiyo mpya hoja binafsi iliyoelezwa kuwa itawasilishwa na Mbunge
wa Kisarawe Seleman Jafo kuhusu kufutwa kwa mafao ya kujitoa kufuatia
marekebisho ya sheria za Hifadhi za Jamii nayo haitawasilishwa kwenye
mkutano huu wa Bunge unaoendelea kama ratiba haitafanyiwa marekebisho.
Hata hivyo, izingatiwe kuwa chanzo cha kufutwa kwa mafao ya kujitoa ni
marekebisho ya sheria za hifadhi ya jamii hivyo ufumbuzi wa kurejesha
fao la kujitoa unapaswa kuwa ni marekebisho ya sheria hatua ambayo njia
ya haraka ya kuifikia ni kuwasilishwa kwa muswada wa sheria ama na
serikali au kamati au mbunge badala ya hoja binafsi.
Hoja binafsi inaweza kuwezesha bunge kujadili na kupitisha maazimio ya
kuitaka Serikali kuwasilisha marekebisho ya sheria au kuishauri na
kuisimamia serikali na mamlaka zake katika utekelezaji wa sheria lakini
sheria itaendelea kuwa palepale mpaka marekebisho yatakapofanywa kwa
kuwasilishwa muswada wa sheria hatua ambayo nimeamua kuanzisha mchakato
wa kuwezesha ichukuliwe.
Wenu katika kuwawakilisha wananchi,
John Mnyika (Mb)
03/08/2012